Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo kuhusu mchakato wa Katiba imewasikitisha.

Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maadili, amani na haki za binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini zote Tanzania, Askofu William Mwamalanga amemshauri Rais John Magufuli kuufufua mchakato huo uliokwama.

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akizungumza jana baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu msimamo wa Kardinali Pengo kwamba Katiba siyo kipaumbele chake, bali huduma za jamii, Mbowe alisema Askofu huyo ni kiongozi wa dini anayepaswa kulinda heshima aliyonayo ndani na nje ya kanisa.

Katika taarifa yake ya kufafanua kauli iliyotolewa na Askofu wa Jimbo la Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi baada ya kukaririwa akisema kwamba Katiba Mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi, Kardinali Pengo alisema hayo yalikuwa maoni yake binafsi siyo msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.

Lakini jana akizungumzia msimamo huo, Mbowe alisema, “Askofu Pengo ni kiongozi wa kanisa, anaheshimika na wananchi ambao si wale anaowaongoza tu lakini kwa kauli yake kuhusu Katiba, imetushangaza na imenisikitisha,”.

Mbowe alisema umefika wakati mchakato wa Katiba uliokwama ukaendelezwa na hasa kuanzia katika rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti, Jaji mstaafu Joseph Warioba.

Mbali ya Mbowe, Askofu Mwamalanga alisema suala la Katiba ni la Watanzania wote na si la mtu au kundi la watu hivyo mchakato huo unapaswa kuhitimishwa na si vinginevyo.

Pia, katibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka ambaye aliomba kutoa maoni yake binafsi kuhusu mchakato huo wa Katiba alisema kinachopaswa kufanyika sasa ni jamii nzima kutafakari ni Katiba ipi ambayo wanaitaka.

Kardinali Pengo Jumamosi iliyopita alinukuliwa akisema kauli iliyotolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi kuwa Katiba mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi ni maoni yake binafsi na si msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.

Amesema hilo alipotoa ufafanuzi kuhusu sitofahamu iliyojitokeza miongoni mwa Watanzania na waumini wa kanisa hilo kutokana na kauli ya Askofu Niwemugizi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *