Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu hatosafirishwa kwenda popote mpaka pale madaktari watakaporuhusu.

Mbowe ameeleza hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari ikiwa imepita siku moja tokea serikali ya Tanzania itoe kauli yake kuwa ipo tayari kumtibia Lissu popote pale duniani kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Ally Mwalimu.

Pia Mbowe amesema wamelazimika kumuwekea ulinzi mkubwa Lissu katika hospitali aliyolazwa kutokana na kuhofia hali ya usalama iliyokuwa imetanda juu ya Mbunge huyo kutokana na shambulio alilofanyiwa na watu waliokosa utu.

Kwa upande mwingine, Mbowe amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na watanzania kwa ujumla kutokuwa na hofu kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu kwani madaktari wameshawahakikishia kuwa Lissu atapona na kurudi kuendelea katika harakati zake alizokuwa anazifanya kama awali.

Tundu Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani mkoani Dodoma baada ya kumalizika kwa kikao cha bunge.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *