Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amethibitisha shamba lake kuvamiwa na viongozi wa serikali ya Wilaya na kuharibiwa miundombinu ya shamba hilo huku akidai anajua yote hayo yanafanyika kutokana na misimamo yake ya kisiasa na kudai hawawezi kumbadili.

Freeman Mbowe amesema hayo leo kupitia mitandao yake ya kijamii huku akikiri wazi kuwa siku ya Alhamisi ya tarehe 7 mwaka huu walipokea barua kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira -NEMC ambayo ilikuwa inadai kilimo wanachofanya kilikuwa kinaharibu mazingira hivyo hawapaswi kuendelea na kilimo hicho.

Mbowe amesema kitendo hicho kilichofanywa na viongozi hao ni kitendo cha kufedhehesha na cha kukatisha tamaa hivyo anasikitishwa sana na kitendo hicho, huku akisema anatambua kuwa yote hayo anayofanyiwa ni kutokana na misimamo yake kisiasa, na misimamo ya chama anachokiongoza.

Mbali na hilo kiongozi huyo amedai kuwa hakuna wingi wa mali zake zinaweza kuharibiwa zikamfanya yeye akapige magoti kama watu wengine wanavyofanya, anadai yeye hawezi kupiga magoti bali atasimama kwenye ukweli na haki siku zote.

Hili ni tukio la pili kwa mwaka huu kutokea kwenye shamba hilo, mwezi wa kwanza mwaka huu serikali ilimtaka kiongozi huyo kusimamisha kilimo kwenye shamba hilo ikidai kuwa lipo kwenye chanzo cha maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *