Mwanamuziki mkongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mbilia Bel leo anatarajiwa kutumbuiza mashabiki wake jijini Nairobi nchini Kenya.

Mbilia Bel aliwasili Nairobi wiki hii kwa mwaliko wa Pamela Olet wa kampuni ya Melamani Productions, lengo kubwa la ziara yake ya wiki mbili nchini Kenya ni kueneza amani na kutumbuiza mashabiki wake na nyimbo zake zilizotia fora kama vile Nakei Nairobi, Eswi Yo Wapi na Nadina alizoimba na marehemu Tabu Ley aliyekuwa kiongozi wa Afrisa International.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC akiwa safarini kuelekea Nairobi kutoka Congo Brazzaville, Mbilia alisema amefurahi kurudi Nairobi baada ya miaka 16.

“Napenda sana mashabiki wangu wa Kenya kwa sababu wananionyesha upendo na wanafurahia nyimbo zangu,” alisema Mbilia Bel ambaye sasa ana umri wa miaka 58 lakini bado ni mrembo tu sana utadhani ana umri wa miaka ishirini hapo.

Nini siri yake ya urembo? “Mimi nala sana maharage na hilo limenisaidia kuwa nilivyo najua wanaume wa Nairobi watanimezea mate lakini hapa nimekuja kwa kazi,” alisema Mbilia Bel kwa utani.

Albamu yake ya mwisho, Signature, ni kuhusu maisha yake yanayoangazia uzuri wake na ubaya.

Mbilia Bel amemsifu sana Tabu Ley kwa kukuuza kipaji chake akiwa mnenguaji akapanda ngazi na akawa mwimbaji.

Baada ya kutumbuiza Nairobi, Mbilia ataelekea Kisumu kuchangamsha mashabiki wake wengi huko Julai tarehe saba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *