Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza baada ya kuwakuta na madawa ya kulevya aina ya Mirungi mafungu 57 yenye ukubwa wa kilogramu 56.75.

Mirungi hiyo ilikuwa imewekwa kwenye mabegi na magunia ambapo watuhumiwa hao walikutwa nayo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi amesema kuwa polisi waliwakamata watuhumiwa hao leo majira ya saa kumi na moja alfajiri katika mtaa wa Mbugani ‘A’ Kata ya Mbugani wilayani Nyamagana.

Kamanda Msangi amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Thomas Zacharia (25), mkazi wa mtaa wa Unguja Mwanza, Ally Athumani (35) mkazi wa Kahama Shinyanga, Nyamurya Elia (35) mkazi wa mtaa wa Unguja Mwanza, na Stanslaus Mapinduzi Elias (41) mkazi wa Tarime.

Kufuatia sakata hilo Kamanda Msangi ametoa wito kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza hususani vijana akiwataka kuacha kujihusisha na biashara za madawa ya kulevya kwani ni kosa kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *