Mawakili wa mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema wamepeleka maombi kuiomba mahakama kuu kanda ya Arusha kumpa mteja wao muda wa kupeleka notisi ya kusudio la kukata rufaa.

Kutokana na hali hiyo, Lema anatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo ili kujua hatima ya maombi ya rufaa yake.

Desemba 2, mwaka huu, mahakama hiyo ilifuta rufaa ya mbunge huyo kutokana na kukatwa nje ya muda, huku mawakili wake wakitakiwa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10.

Hatua hiyo ilikuja baada ya uamuzi wa maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya chini kutupwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sekela Moshi, Novemba 11, mwaka huu.

Lema ambaye anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika Gereza Kuu la Kisongo, mjini Arusha, alikamatwa Novemba 2, mwaka huu, nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa mahakamani mjini Arusha, Novemba 8, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *