Jeshi la Polisi limekusudia kuwachukulia hatua za kisheria wasanii wa kundi la Orijino Komedi kwa kuvaa sare zinazofanana na sare za jeshi hilo kwenye harusi ya mchekeshaji mwenzao Emmanuel Mgaya a.k.a ‘Masanja Makndamizaji’ wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Kupitia taarifa ya vyombo vya habari msemaji wa jeshi la Polisi, ACP Advera John Bulimba ameeleza kwamba jeshi hilo litawachukulia hatua za kisheria wachekeshaji hao kwasababu kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba kwa mujibu wa sheria ya kanuni ya makosa ya jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178 (1) kinachozungumzia makosa juu ya sare za majeshi ya ulinzi na usalama kinabainisha wazi kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyoto ambaye si mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvalia mavazi hayo au yanayoshabihiana mpaka kupata ruhusa kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Vile vile ACP Advera alitoa onyo kwa wananchi wanaovalia sare hizo au zinazofanana na majeshi yote nchini kuacha mara moja kwani wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria dhidi yao huku akiwataka wanaomiliki mavazi ya aina hiyo kuyasalimisha katika vituo vya Polisi vilivyopo karibu na maeneo yao.

Joti, Wakuvanga na Mack Regan walivalia mavazi hayo na kuingia nayo ukumbini wakati wa sherehe ya harusi ya mchekeshaji mwenzao Masanja Mkandamizaji iliyofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *