Matokeo ya mchezo wa ligi kuu Tanazania Bara kati ya Ndanda FC na Simba hayatafutwa hata kama itabainika kuwa Simba iliwachezesha wachezaji ambao hawakuwa na vibali vya kucheza ligi ya Tanzania.

 

Katika mchezo huo Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0 na kuondoka na point 3, huku ikiwachezesha wachezaji wake wawili iliyowasajili hivi karibuni kutoka nchini Ghana, ambao ni kiungo James Kotei na golikipa Daniel Agyei.

 

Baada ya mchezo huo klabu ya Ndanda iliwasilisha malalamiko katika bodi ya ligi ikidai kupewa point 3 za mezani kwa madai ya Simba kuwatumia wachezaji ambao hawakustahili.

 

Akitolea ufafanuzi madai hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmad Yahya amesema kuwa bodi hiyo haihusiki na masuala ya usajili, na kama Ndanda wana malalamiko wanapaswa kuyapeleka katika kamati ya sheria na hadhi za wachezaji.

 

Mwenyekiti huyo pia hakusita kuchambua kanuni za ligi akisema kuwa kwa mujibu wa kanuni hizo endapo itabainika kuwa Simba imewatumia wachezaji wasiostahili, matokeo ya uwanjani hayataathirika, isipokuwa wachezaji wenyewe wanaweza kupewa adhabu ikiwa ni pamoja na kufungiwa au kupigwa faini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *