Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki ameagiza kufutwa kwa mashirika manne yasiyo ya serikali kutokana na kufanya kampeni chafu za kupiga vita Mlima Kilimanjaro na uchochezi wa kuchafua sifa ya nchi.

Ametoa agizo hilo jana wakati wa kukabidhi Bendera ya Taifa wakati wa kuwaaga wapanda mlima wanaoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Jenerali mstaafu George Waitara anayeongoza baadhi ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wanahabari nchini.

Sadiki amesema mashirika hayo yamekuwa yakifanya kampeni chafu za uchochezi kuwa serikali kwa kushirikiana na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), imekuwa ikiwanyanyasa wananchi katika matumizi ya eneo tengefu la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro linalojulikana kwa jina la Nusu Maili.

Amesema serikali ya mkoa imekamata machapisho yenye uchochezi pamoja na fomu ambazo zinawataka wananchi kujiorodhesha na kusaini ili kukubali kuwa wanateswa na serikali pamoja na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchapisha kwenye mashirika mengine ya kimataifa kuwa Tanzania inakandamiza haki za binadamu.

Amesema baadhi ya mashirika hayo yamesajiliwa nchini Japan, lakini yamechukua jukumu la kuwasemea wananchi wa Kilimanjaro, hivyo uongozi wa mkoa umekaa vikao vyote na kinachosubiriwa kwa sasa ni mamlaka husika iliyozisajili kuzifutia usajili wao, kwa sababu zinachafua sifa ya taifa na utalii wa Mlima Kilimanjaro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *