Nchi tano zinatarajia kushiriki mashindano ya Michuano ya Mabingwa ya mchezo wa ngumi yanayotarajiwa kuanza Desemba 09 mwaka huu jijini Dar es salaam.

Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Nchini BFT Mutta Rwakatare amesema, wamejiandaa vizuri ikiwa ni pamoja na kupambana na changamoto za kiuchumi ambazo bado zinaendelea kujitokeza katika chama.

 

Rwakatare amesema mashindano hayo yatakuwa ya wazi ili kuweza kuhakikisha wanapata wadau ambao wataweza kuusaidia mchezo huo kuweza kusonga mbele zaidi.

 

Rwakatare amesema, mashindano hayo pia yatasaidia kupata mabondia watano wenye vipaji vizuri ambao wataelekea nchini Cuba wakiongozana na kiongozi mmoja kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya mashindano yajayo ya Olimpiki yatakayofanyika mwaka 2020 jijini Tokyo nchini Japan ambayo ni ofa kutoka kamati ya Olimpiki nchini TOC.

 

Rwakatare amezitaja nchi zilizothibitisha kushiriki katika mashindano hayo ambayo yatafikia tamati Desemba 15 kuwa ni Cameroon, Kenya ambayo italeta timu mbili: moja kutoka Mombasa na nyingine kutoka Nairobi, Uganda, Rwanda, Burundi na wenyeji Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *