Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji anatarajiwa kukabidhiwa rasmi timu hiyo baada ya mchezo wao wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba Oktoba Mosi mwaka huu.

Bodi ya Wadhamini ya Yanga chini ya Fatuma Karume na Francis Kifukwe imeridhia kumkodisha rasmi Manji timu hiyo kwa miaka 10 kama alivyoomba kupitia mkutano wa dharura wa wanachama wa klabu hiyo uliofanyika Juni 11 mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam.

Manji aliomba apewe klabu kwa miaka 10 na katika kipindi hicho atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu, huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama ambapo pia katika kukodishwa huko timu ya soka na nembo ya klabu zote zitakuwa chini ya kampuni zake.

Hivi karibuni Kifukwe aliiambia HabariLeo kuwa wamesharidhia kumkabidhi Manji timu na kwamba bado kuna vitu vidogo vidogo wanakamilisha.

Lakini hata hivyo jana mmoja wa vigogo wa klabu hiyo aliihakikishia HabariLeo kuwa Manji atakabidhiwa timu hiyo baada ya mchezo na mahasimu wao. Hata hivyo, Kifukwe jana alipoulizwa kuhusu kumkabidhi Manji timu baada ya Oktoba Mosi alisema “Kwa upande wetu tumeshamaliza, suala hilo kwa sasa lipo mikononi mwa Kamati ya Utendaji ya Yanga, wao ndio wanapaswa kuzungumzia suala hilo”.

Kwa upande wa Katibu wa Yanga, Baraka Deusdetit alipoulizwa kuhusiana na suala hilo amesema: “Hilo suala ni la Bodi ya Wadhamini vipi lirudi kwenye Kamati ya Utendaji, nadhani bodi ya wadhamini ndio wanapaswa kuzungumzia suala hilo, inawezekana mchakato bado haujakamilika ndio maana wanasita kuuzungumzia, ukikamilika utawekwa wazi hakuna cha kuficha,”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *