Aliyekuwa mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amevuliwa nafasi ya udiwani wa kata ya Mbagala Kuu baada ya kushindwa kuhudhuria vikao kutokana na kukabiliwa na kesi Mahakama ya Kisutu.
Manji amepoteza sifa ya kuwa Diwani wa Kata hiyo kutokana na kutohudhuria vikao zaidi ya sita na vikao vya kamati vya maendeleo ya halmashauri ya Temeke zaidi ya vitatu.
Hayo yamesemwa leo na Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Chaurembo katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuvuliwa udiwani kwa kiongozi huyo.
Meya Chaurembo ameongeza kwa kusema kuwa amemwandikia barua Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene kuhusu suala hilo ili aweze kupanga uchaguzi mwingine.
Manji ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Quality Group anakabiliwa na kesi ya zaidi ya mbili moja ikiwa ni matumizi ya dawa za kulevya na nyingine uhujumu uchumi.
Kwasasa Manji yupo ndani kutokana na kesi hizo ambapo imepelekea mpaka kushindwa kuhudhuria viako vya udiwani kwa ajili ya maendeleo ya kata hiyo ya Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam.