Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Salma Kikwete,  amemshukuru  Rais  Dk. John  Magufuli  kwa kumwona na kumteua kuwa  mbunge  wa Bunge  la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania.

Salma ambaye pia ni Mjumbe  wa Halmashauri Kuu ya CCM akitokea Wilaya ya Lindi Mjini, alitoa shukrani  hizo wakati alipopewa nafasi ya kutoa  salamu kwa wakazi wa Kata ya Ngapa  waliohudhuria  ziara ya Rais Magufuli ya  kukagua mradi wa maji wa eneo hilo.

Salma ambaye yupo mkoani Lindi, alijitokeza jana katika ziara ya Rais Dk. Magufuli mkoani humo ambapo mbali na kutoa shukrani hizo alisema tatizo la  maji katika Manispaa ya Lindi limekuwa  kero ambayo inanyima utulivu  kwa  watendaji  na viongozi wa wilaya na mkoa huo kwa ujumla.

Katika hilo alisema kwa nafasi aliyopewa atahakikisha anawawakilisha vyema wananchi wa Lindi na atashirikiana na wabunge wa mkoa huo kutatua kero ya maji.

Uteuzi huo wa Salma umekuja ukiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja tangu jina lake litajwe na kuhusishwa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *