Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema ataunda kikosi kazi kitachoshirikisha Jeshi la Polisi kukabiliana na uvuvi haramu wa mabomu unaofanywa na wavuvi katika pwani ya Kigamboni.

Kuundwa kwa kikosi kazi hicho kunafuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi waliyoyatoa kwa Makonda kuwa kuna baadhi ya wavuvi wanatumia mabomu kuvua samaki katika eneo hilo.

Amepiga marufuku uvuvi huo na kusema kwa kushirikiana na Polisi watafanya doria katika bahari na kwamba wakibaini mtu anaendesha uvuvi wa mabomu atachukuliwa hatua.

Makonda amesema endapo wazee wa zamani wangetumia milipuko na mabomu kuvua samaki jamii isingefika hapa ilipo, hivyo ni vyema kufikiria kizazi kijacho na cha baadaye.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaagiza wenyeviti wa mitaa katika Manispaa ya Kigamboni kuhakikisha wanakuwa walinzi katika mitaa.

Sirro ametoa kauli hiyo wakati akijibu maswali ya baadhi ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Manispaa ya Kigamboni na kuelezea kero zao kuhusu Jeshi la Polisi, ikiwemo ya kutokupatiwa msaada wa haraka wa panapotokea uhalifu kwa madai ya kukosa mafuta ya gari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *