Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amevituhumu vyombo vya habari nchini kuwa vinadhoofisha maendeleo ya wananchi kwa kuminya haki yao ya kupata habari.

Makonda alitoa madai hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati akihojiwa na Kituo cha Star TV kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ya mkoa baada ya kutimiza mwaka mmoja.

Amesema baadhi ya vyombo vya habari vimepotoka kwa kumwadhibu yeye kwa madai ya kuminya uhuru wa vyombo hivyo baada ya kudaiwa kuvamia kituo cha Clouds Tv.

Makonda amesema kuwa hatua hiyo imegeuka kuwa adhabu kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwani wanaokosa taarifa ni wao.

Mkuu wa mkoa huyo amesema kuwa hakufanya uvamizi kama inavyodaiwa na waandishi bali alikwenda Clouds kama nyumbani kwa rafiki zake na kuwa madai hayo yametengenezwa ili kufifisha vita dhidi ya madawa ya kulevya.

Amesema kutokana na waandishi kumbania habari zinazohusu wananchi wake, wanakosa kujua maendeleo ya mkoa wao aliyofanya katika kilimo, ujenzi, miundombinu, afya.

Makonda hakuweza kufafanua zaidi juu ya alichokuwa ameandaa kama makala maalum ya mafanikio yake kwa mwaka mmoja sasa akiwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.

Makonda alisema alikuwa anamaliza kuandaa makala maalum ambayo ingerushwa katika vyombo mbalimbali vya habari na tayari baadhi ya vyombo vilishaanza kuiulizia viitoe.

Pia amesema makala hiyo haikuweza kutoka kufuatia kuzushiwa kuwa alivamia kituo cha Clouds TV na kisha kufungiwa na waandishi wa habari kutoa habari zinazohusu kazi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *