Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametakiwa kufika mbele ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya  Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madai ya kudharau Bunge.

Maamuzi hayo ni sehemu ya maazimio manne ya  Bunge yaliyopitishwa dhidi ya viongozi wanaoteuliwa na Rais hasa wakuu wa mikoa na wilaya, ambapo azimio lingine ni kumtaka Waziri wa TAMISEMI kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutoingilia majukumu yasiyo yao.

Hatua hiyo inafuatia hoja iliyotolewa bungeni hapo na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, kufuatia kauli inayodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa wa  Dar es Salaam Paul Makonda inayodaiwa kuwa ni dharau kwa Bunge.

Pia Mwita amedai kuwa viongozi mbalimbali hasa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia madaraka yao vibaya kiasi cha kuingilia majukumu yasiyo yao, na wakati mwingine kuingilia majukumu ya Bunge, na kutolea mfano Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Alexander Mnyeti.

Baada ya hoja yake kukubaliwa na Mwenyekiti wa kikao hicho Mh Andrew Chenge, wabunge wameijadili ambapo wabunge kadhaa akiwemo Ester Bulaya, Zitto Kabwe, Saed Kubenea na Joseph Musukuma wamepata fursa ya kuchangia ambapo kwa kiasi kikubwa wote wameonesha kukerwa kauli hiyo inyodaiwa kutolewa na Paul Makonda, pamoja na utaratibu wa wabunge kukamatwa bila utaratibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *