Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kumhamisha Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dk Aziz Msuya kwa madai ya kuwepo kwa ubadhirifu wa dawa huku madaktari na wauguzi wakidaiwa kuwauzia wagonjwa dawa hizo.

Uamuzi wa Makonda umefika baada ya wananchi wa Tandale jijini Dar es Salaam kudai Kituo cha Afya cha Tandale kutokuwa na dawa huku wakilazimika kununua kutoka kwa madaktari na wauguzi.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema kuwa hayo ni matokeo ya kutokufuatilia na kwamba Dk Msuya alikuwa anakaa ofisini kwani alishapata taarifa ya uwepo wa wizi wa dawa unaofanywa na madaktari.

Akizungumzia hatua hiyo, wakati wa ziara ya Makonda ya siku 10 ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi eneo la Shule ya Msingi Tandale, Dk Msuya alisema ana uhakika hakuna upungufu wa dawa huku akibainisha kama kuna upungufu huo achukuliwe hatua.

“Mkuu wa Mkoa mimi nina uhakika kama kuna upungufu wa dawa mtu akathibitisha kweli nina taarifa na sijachukua hatua basi nichukuliwe hatua,” alisema Dk Msuya.

Baada ya kauli hiyo, Makonda alimtaka Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Hapi kuthibitisha taarifa hizo ambapo alisema hizo ni changamoto za daktari huyo kutokuwa mfuatiliaji katika vituo hivyo vya afya, kwani wapo baadhi ya madaktari wasiokuwa waaminifu wanauza dawa kwa wagonjwa kinyume na taratibu za serikali.

“Na hivi tunavyozungumza tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanazo taarifa hizo, sasa mimi nashangaa kwa nini Mganga wa Wilaya hana,” alisema Hapi. Kufuatia hali hiyo, Msuya alisema taarifa hiyo haijafika katika ofisi yake.

Lakini Makonda alisema Rais hayupo tayari kushuhudia majibu aliyotoa Msuya na kushindwa kutimiza majukumu yake.

“Kuanzia sasa ninaelekeza Wizara ya Tamisemi chini ya Katibu Mkuu kukung’oa madaraka yako na kukuhamishia mkoa mwingine wa kwenda watakupangia kazi nyingine ukafanye. Unatoa taarifa za upungufu wa dawa huku kukiwa na ubadhirifu wa dawa na mnashirikiana, ‘bai bai’ kwenye mkoa wangu,” alisema Makonda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *