Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema rushwa ni miongoni mwa vitu vinavyoharibu maendeleo na kwamba kukithiri kwa vitendo hivyo katika nyanja mbalimbali kunasababisha wananchi kukosa imani na serikali yao.

Samia ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa Kimataifa wa kubadilishana uzoefu katika vita dhidi ya rushwa ambapo amesema, rushwa inatakiwa kushughulikiwa kuanzia kwenye kiini na kwamba serikali inalihakikisha hilo.

“Rushwa ni uovu ambao umeendelea kuharibu nyanja zote za maendeleo ya binadamu. Rushwa hudhoofisha utawala wa sheria, hivyo huharibu uaminifu wa umma kwa serikali,” alisema Samia.

Alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imejidhatiti katika mapambano dfhidi ya rushwa na kwamba tayari kuna mikakati mbalimbali iliyowekwa kwa ajili ya vita hiyo ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu (NACSAP III).

Mkutano huo unafanyika nchini kutokana na ombi la Rais John Magufuli kwa Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim kusaidia Tanzania katika kuimarisha utawala bora. Mkutano huo unaelezwa utakuwa msaada kwa Tanzania katika vita dhidi ya rushwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *