Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema asilimia 61 ya nchi ina hatari ya kuwa jangwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uharibifu wa mazingira haswa uchomaji mkaa.

January aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifanya ziara ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Erik Solheim ya kuangalia hali ya mazingira katika dampo la Pugu Kinyamwezi na eneo la mkaa Ubungo Riverside.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia jinsi wanaweza kushirikiana na kuhakikisha taka zinageuzwa na kuwa fursa.

Akizungumza na kikundi cha kinamama cha biashara ya mkaa Riverside, January alisema watashirikiana na UNEP na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wanapunguza shughuli za uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji mkaa.

Kwa upande mwingine amezungumza kuhusu dampo la Pugu, Makamba amesema wanataka kushirikiana kufanya taka kuwa malighafi sambamba na kuzitumia kuzalisha umeme.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *