Watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.

Majambazi hao walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya Toyota Rav4 yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Richard Charles.

Kwenye gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China, aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.

Kwa mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha hizo benki eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao wakiwa na pikipiki aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni wakisubiri taa ziwaruhusu kupita kutoka barabara ya Mandela.

Charles alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi la fedha lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa bastola kabla ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha hizo na kutokomea nazo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *