Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetoa siku saba kwa majambazi wote waliowahi kutumikia vifungo na kuachiwa kwa kumaliza vifungo au rufaa, wajisalimishe kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lucas Mkondya wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mkondya amesema lengo la kuwaita majambazi hao ni kutaka kupanga utaratibu mzuri ili waone kama baada ya vifungo vyao, wamebadilika na wanajihusisha na shughuli gani kwa sababu walikuwa ni majambazi sugu na walifanya matukio.
Mkondya aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa, kutoa taarifa kama kuna majambazi katika maeneo yao ambao wamechiwa ili polisi wawafuatilie kikamilifu.
Katika tukio jingine, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 44 wa wizi wa vifaa vya magari pamoja na vifaa hivyo vya magari.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na operesheni maalumu, ambayo inalenga kuwakamata wezi wa vifaa mbalimbali vya magari, ikiwa ni pamoja na wanunuzi wa vifaa hivyo katika sehemu mbalimbali za jiji hili.
Aliongeza kuwa operesheni hiyo iliyoanza Julai 18, mwaka huu na katika operesheni hiyo ambayo endelevu, watuhumiwa hao walikamatwa na baada ya kupekuliwa katika maduka yao walikutwa na vifaa mbalimbali vya magari.
Katika mahojiano na watuhumiwa wote waliokamatwa, wapo walioshindwa kuvitolea maelezo vifaa hivyo ni namna gani na wapi vifaa hivyo wamevipata huku baadhi ya vifaa vikionesha kuwa vimefunguliwa kutoka kwenye magari mengine kwani vimekutwa na namba za magari.
Aidha, jeshi hilo linawashukuru wananchi kwa kutoa taarifa na kuwataka wafanyabiashara wa vifaa vya magari kufuata sheria zinazowawezesha kufanya biashara hiyo kihalali.