Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa amesema serikali itahakikisha inawasaka wote waliohusika na upotevu wa mali za kiwanda cha chai cha Lupembe na kuwachukulia hatua.

Pia amewataka wawekezaji mbalimbali waliomilikishwa viwanda wahakikishe wanafuata kanuni na sheria ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na wananchi waweze kupata tija.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea Kiwanda cha Chai cha Lupembe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.

Mali za kiwanda hicho vikiwemo vipuri na vyombo vya usafiri yakiwemo malori na magari madogo 17 vilipotea baada ya Ushirika wa wakulima wa chai Muvyulu kuvamia kiwanda.

Kiwanda hicho kinakabiliwa na mgogoro kati ya mwekezaji wa kiwanda hicho, Lupembe Tea Estate na Ushirika wa Wakulima wa Chai Muvyulu ambao ameahidi kuitafutia ufumbuzi.

Alisema serikali itayafanyia kazi maelezo yote yaliyotolewa na uongozi wa kiwanda hicho pamoja na ya wanaushirika na kisha itayatolea ufafanuzi wakati kiwanda kikiendelea na kazi.

Majaliwa alisema serikali itahakikisha mwenye haki anapata haki yake na haitakubali kuona kiwanda hicho kikisimamisha uzalishaji. Pia inafuatilia mwekezaji huyo alipataje kiwanda.

Waziri Mkuu ameendelea na ziara yake mkoani Njombe baada ya kuikatiza Januari 22, mwaka huu na kwenda mkoani Dar es Salaam kwa shughuli za kikazi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *