Majaliwa: serikali imelipa Sh bilioni 29 kwa watumishi wa umma wakiwemo walimu

0
265

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali imelipa jumla ya Sh bilioni 29 kwa watumishi mbalimbali wa umma wakiwemo walimu, ikiwa ni sehemu ya madeni yao.

Ametoa kauli hiyo wakati akizindua vyumba vitatu vya kisasa vya madarasa katika Shule ya Sekondari Iwawa iliyoko wilayani Makete.

Waziri Mkuu alisema serikali imedhamiria kumaliza madeni ya watumishi hao, ambapo hadi kufikia Novemba mwaka jana, jumla Sh bilioni 29 zililipwa kwa watumishi 31,000.

Amesema kwa sasa serikali imejipanga kuhakikisha hakuna madeni mapya yanayozalishwa hivyo amewataka watumishi wa umma na wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali. Hata hivyo, alisema serikali inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

Amesema nyumba hizo za walimu zinazojengwa katika maeneo mbalimbali hususan ya vijijini ni za kisasa ambazo zinalenga kuwaondolea changamoto ya makazi. Majaliwa alisema serikali inafanya jitihada za dhati za kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu kwa kuwa elimu ni kichocheo cha maendeleo ya jamii.

Mkuu wa shule hiyo, Novatus Msivala, aliishukuru serikali kwa kugharamia ujenzi wa vyumba hivyo vitatu vya madarasa na matundu 10 ya vyoo pamoja na uingizaji wa maji kwenye vyoo na utengenezaji wa madawati 46.

Amesema ujenzi huo umegharimu Sh milioni 95 ambao utasaidia kupunguza msongamano kwa wanafunzi. Kwa sasa serikali na wananchi wanaendelea kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu.

LEAVE A REPLY