Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga amesema suala la mageuzi katika Umoja wa Mataifa ni muhimu.

Amesema wameomba Afrika ipewe viti viwili vya ziada katika viti vya mzunguko na viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ameyasema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya miaka 71 ya Umoja wa Mataifa (UN), yatakayofanyika Oktoba 24 mwaka huu, Dar es Salaam.

Amesema wenye kura ya kudumu ni 15, lakini watano ndiyo wanabaki tangu mwaka 1945 kwa kuwa ndiyo walikuwa washindi kwenye vita kuu na wenye uwezo.

Amesema kwa sasa wanachama wameongezeka, hivyo katika kura ya turufu pia wanapaswa kuongezwa kwa kuwa idadi ya Waafrika pia imeongezeka.

Amesema mazungumzo ya mageuzi hayo yameendelea kwa miaka 10 sasa, ingawa kwa Afrika bado kuna mkanganyiko nani wapewe kura mbili za turufu na nchi zilizokuwa zimeonesha kutaka nafasi hiyo ni Nigeria, Afrika Kusini na Misri.

Akizungumzia maadhimisho hayo ambayo yamebeba ujumbe wa “Uwezeshaji wa Vijana Tanzania kufikia malengo ya dunia” yatafanyika huku kukiwa na malengo mapya ya dunia ya maendeleo endelevu yaliyolenga kuondoa umaskini.

Amesema maadhimisho hayo yanaonesha ni kwa namna gani pande zote zipo tayari kutekeleza mipango ya maendeleo ya UN nchini, yenye lengo la kusaidia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.

Pia amesema Tanzania inaiunga mkono UN ikifanya kazi kama taasisi moja na kutaka itengenezwe sera kuhakikisha wananchi wananufaika na ushirikiano wa Tanzania na Umoja huo wa Mataifa.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Mashirika ya UN nchini, Chinasa Kapaya, alisema Tanzania na UN zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa miongo mingi, hivyo nchi hiyo inapoelekea kwenye uchumi wa kati inapaswa kubadilika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *