Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru kwa mara nyingine mshtakiwa Harbinder Sethi akatibiwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ndani ya siku 14.

Korti imesema iwapo hilo halitatekelezwa, mkuu wa gereza afike mahakamani kujieleza. Sethi yupo mahabusu katika Gereza la Segerea.

Amri hiyo ya mahakama imetolewa baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kudai kesi ilipangwa leo Ijumaa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba shauri lipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, wakili Joseph Makandege anayemwakilisha Sethi alieleza kuwa kumekuwepo mfululizo wa amri za Mahakama zikiagiza mteja wake akapatiwe matibabu na kufanyiwa uchunguzi Muhimbili.

Amesema kwa kuwa upande wa mashtaka umekaidi amri za Mahakama, anaomba itoe adhabu inayostahili.

Makandege amesema kitendo cha upande wa mashtaka cha kutotekeleza amri za Mahakama kinasigana na kukiuka mamlaka aliyopewa Mkurugenzi wa Mashtaka .

Ameomba Mahakama itoe adhabu stahiki kwa kuwa hilo linaonyesha dhahiri kuwa mashtaka yaliyopo ni ya hila yenye lengo la kuwaadhibu washtakiwa na hasa mshtakiwa wa kwanza Sethi kabla hawajahukumiwa.

 Wakili Makandege ameiomba Mahakama iitupilie mbali hati ya mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa ili Sethi apate wataalamu wa matibabu yake katika hospitali ikiwemo Muhimbili.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai tatizo limeshajitokeza katika utekelezaji wa amri za Mahakama.

Swai amedai Magereza wamekuwa wakiwatibu wafungwa na mahabusu hata pasipokuwa na amri ya Mahakama.

Amesema kilichojitokeza ni utaratibu wa kumpeleka Sethi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hakimu Huruma Shaidi amesema ni lazima amri za Mahakama zifuatwe. Ameahirisha kesi hadi Oktoba 13.

Amesema hadi siku hiyo, Sethi awe ameshapata matibabu na iwapo atakuwa hajapatiwa, mkuu wa gereza alipo afike mahakamani kujieleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *