Kesi ya wizi wa Sh bilioni 3.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Jayantkumar Patel na wenzake watatu imesimamishwa.

Amri ya kusimamisha kesi hiyo imetolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ilipokuwa inasikilizwa kesi hiyo.

Jopo la mahakimu watatu likiongozwa na Hakimu Ignas Kitusi lilitoa amri ya kusimamisha kesi hiyo jana, hadi kesi yao ya kikatiba iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu itakapotolewa uamuzi.

Hatua hiyo inatokana na maombi yaliyowasilishwa ya kusimamishwa kwa kesi hiyo yaliyowasilishwa na mawakili wa upande wa utetezi, Martin Matunda na Mabere Marando wakidai mshitakiwa alifungua kesi Mahakama Kuu akidai kuvunjiwa haki ya kikatiba na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya IPP, Reginald Mengi.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa, Aprili 23, mwaka jana, Mengi alitumia vyombo vya habari kumhukumu Jeetu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ kabla Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi dhidi ya mteja wao haijatoa hukumu.

Mawakili hao wanadai wamefungua kesi hiyo wakiomba tafsiri ya kisheria kwa kuwa wanaamini haki ya mteja wake imevunjwa.

Mbali na Mengi, Jeetu amefungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ambao anadai kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao baada ya Mengi kumhukumu kupitia vyombo vya habari.

Katika kesi nyingine, mshitakiwa huyo amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ilioamuru majalada ya kesi zinazomkabili na wenzake, kurudi Mahakama ya Kisutu ili ziendelee.

Jeetu pamoja na Devendra Patel, Amit Nady na Ketan Chohan wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha kutoka kwenye Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu, zili funguliwa Novemba mwaka juzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *