Mahakama kuu kitengo cha biashara, imetoa siku saba kwa Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi kuwasilisha hati ya kiapo kujieleza kwa nini asifungwe jela kwa kushindwa kutekeleza hukumu inayohusu malipo ya Sh bilioni 1.2.

Jaji Mfawidhi, Amir Mruma ametoa amri hiyo leo baada ya kukubali ombi la Dk Mengi kujieleza kwa njia ya kiapo, lililowasilishwa na wakili wake, Deogratius Ringia.

Mengi anatakiwa kujieleza kutokana na kushindwa kutekeleza hukumu iliyomtaka kuwalipa wafanyabiashara watatu, Muganyizi Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles Mgweo, Dola za Marekani 598,750 sawa na Sh bilioni 1.2.

Jaji Mruma amesema Mahakama imekubali ombi la Mengi kujieleza kwa njia ya kiapo na kuamuru awasilishe maelezo hayo ndani ya siku saba kuanzia jana na upande wa walalamikaji wajibu ndani ya siku saba baada ya kupokea kiapo hicho.

Jaji Mruma amesema bado kuna nafasi ya Mengi kufika mahakamani na kujieleza zaidi kama kutakuwa na jambo ambalo litakuwa linahitaji afike kueleza.

Mengi alitakiwa kuwalipa wafanyabiashara hao, kutokana na mgogoro wa malipo ya uuzwaji wa hisa katika Kampuni ya Douglas Lake Minerals Ltd ambayo kwa sasa inaitwa Handeni Gold Inc.

Hatua ya Mengi kutakiwa kujieleza inatokana na wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi ya kukazia hukumu iliyotolewa Januari 28, mwaka huu na Jaji Agathon Nchimbi wa mahakama hiyo.

Katika hati ya kiapo ya wafanyabiashara hao, inadaiwa walifungua kesi dhidi ya Mengi na Kampuni ya K.M. Prospecting Limited, wakidai malipo yaliyokuwa yamebakia ya dola 428,750, 100,000 na 70,000, kwa kila mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *