Viongozi saba wa chama cha Madaktari chini Kenya (KMPDU) wamehukumiwa jela mwezi mmoja baada ya kukaidi agizo la Serikali la kumaliza mgomo wa madaktari nchini humo.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya masuala ya wafanyakazi nchini Kenya kutokana na viongozi hao kushindwa kumaliza mgomo wa madaktari ambao umedumu zaidi ya miezi miwili nchini na kuathiri sekta ya afya.

Jaji Hellen wa mahakama hiyo Wasilwa amesema viongozi hao hawajatoa sababu ya kutosha kuonesha ni kwa nini hawajamaliza mgomo huo mpaka kupelekea maafa makubwa kwa wagonjwa kwa kukosa huduma.

Jaji Wasilwa alikuwa aliwapa viongozi hao muda wa wiki mbili kumaliza mgomo huo, na baadaye akawaongezea siku tano lakini wameshindwa kufanya hivyo.

Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali ya Kenya kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara lakini Serikali imeshindwa kufanya hivyo.

Wamekataa mshahara walioongezewa na serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule walioafikiana mwaka 2013.

Karibu madaktari na wauguzi 5000 kutoka hospitali 2000 za umma, walianza mgomo wiki ya kwanza ya mwezi Desemba mwaka jana na wagonjwa wamekuwa wakikosa matibabu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *