Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli amezuia serikali kupeleka chakula cha msaada wilayani Misenyi mkoani Kagera kwa madai kuwa wilaya hiyo haina sababu ya kukumbwa na tatizo la njaa.

Rais Magufuli amekataa serikali kupeleka chakula cha msaada katika wilaya hiyo na kusema haikubaliki kwa eneo hilo lenye mvua za kutosha na hali nzuri ya kilimo na kwamba haiwezekani kulia njaa wakati kuna uwezekano wa kuzalisha kwa ajili ya chakula.

Amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha kata ya Ishozi Wilayani Misenyi Mkoani Kagera ambapo yupo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kukagua maendeleo mbalimbali.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli, amesema kuwa serikali haitaweza kujenga makazi ya kila mwathirika wa tetemeko mkoani Kagera kwa kuwa ina jukumu la kujenga miundombinu itakayokuwa na manufaa kwa jamii nzima kama Zahanati, Shule na barabara.

Amesema kuwa kuna baadhi ya watu ambao nyumba zao hazikuharibika kiasi kikubwa lakini wakadanganywa na baadhi ya watu kuwa watajengewa hivyo wakazibomoa kwa kutaka kujengewa nyumba mpya.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *