Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wa majeshi nchini kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa madawa ya kulevya bila ya kujali nafasi zao, na umaarufu wao.

Rais Magufuli amesema hakuna cha mtu maarufu wala mtoto wa kiongozi, yeyote akikamatwa afikishwe mahakamani na kuagiza mahakama kuharakisha kutoa hukumu zinazohusu dawa za kulevya.

Pia amesema hata kama ni mke wake, naye anatajwa kuhusika na dawa za kulevya, akamatwe haraka na apelekwe mahakamani.

Vile vile Rais Magufuli amekiri kuwa anafahamu kuna watu walikuwa wanampigia simu IGP Ernest Mangu na kumpa ushauri juu ya mambo ya madawa ya kulevya, hivyo Rais amesema kama angejaribu kuwasikiliza basi leo asingekuwa na hiyo nafasi tena.

Kauli hii ya Rais Magufuli inakuja ikiwa ni siku chache tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda atangaze vita dhidi ya watu wanaohusika na dawa za kulevya akianza kwa kutaja majina yakiwemo ya askari na ya wasanii maarufu wa muziki na filamu akiwemo Wema Sepetu, Chid Benz, Vanessa Mdee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *