Mkurugenzi wa Ushauri wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Edwin Nnunduma amesema kuwa majengo katika mradi wa nyumba za makazi Magomeni yanajengwa kwa teknolojia ambayo imezingatia uwezo wa wakazi wake kuwa na majiko yanayoweza kutumia kuni na mkaa.

Mkurugenzi huyo amesema hayo wakati akimpa taarifa ya utekelezaji Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyefika katika eneo la mradi Magomeni Kota jana, kuona maendeleo yake.

Eneo hilo lilikuwa linakaliwa na watu 600 wa hali ya chini ambapo sehemu kubwa ya nishati wanayotumia inatokana na mkaa na kuni. Mhandisi huyo alisema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itahusisha majengo matano ya makazi.

Mhandisi Nnunduma alisema mradi huo ambao unajengwa kwa awamu tofauti utahusisha ujenzi wa nyumba za makazi, maduka makubwa na ya kisasa pamoja na ofisi na kwamba awamu ya kwanza inatarajia kukamilika Oktoba mwakani.

Mhandisi huyo alisema awamu ya kwanza iliyoanza Oktoba mosi, mwaka huu inahusisha ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo hilo ambayo inatarajiwa kukamilika Oktoba mwakani.

Akiwa katika mradi huo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wataalamu wa ujenzi wa mradi kutumia utaalamu wao vizuri na kukamilisha kazi kwa wakati. Waziri Mkuu aliwataka wataalamu hao waendelee kufanya kazi hiyo kwa kufuata misingi ya weledi wa taaluma yao kwani Serikali inawaamini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *