Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida amewataka wanachama wa chama hicho kubadilika kifikra ili kuendana na muundo wa sasa.
Akizungumza jana wakati wa kuwapokea wanachama wapya katika Tawi la Kimanga Kuu mwenyekiti huyo amesema mabadiliko hayo yataleta mageuzi makubwa ndani ya chama hicho.
Wanachama hao ambao wamehama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ni Mwalimu Anthony Gella, Joel Sasabo, Daniel Ndengetu, Samuel Lyimo na Joseph Chausi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Assah Simba, alisema Kata ya Kimanga licha ya kusumbuliwa na upinzani pia ilikuwa inaongoza kwa kuwa na migogoro ya ndani.
Awali Mwalimu Gella ambaye alikuwa Katibu wa Kata ya Kimanga, alisema amehama Chadema kutokana na kukerwa na tabia ya viongozi wa wilaya na mkoa aliodai kuwa ni wababe, wabaguzi na kwamba wanaikanyaga katiba.
Kwa upande wake Sasabo ambaye alikuwa Katibu wa Baraza la Wazee Jimbo la Segerea, alisema anarudi CCM baada ya kuona hivi sasa kuna mwanga kwani mambo mengi waliyokuwa wakiyapigania Rais Magufuli anayatekeleza.