Kocha mpya wa Yanga, George Lwandamina amechimba mkwara mzito na kusema atakuwa mkali kwa wachezaji wazembe kwenye klabu hiyo.

Lwandamina ametangazwa rasmi kuwa kocha mpya wa klabu hiyo na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa klabu hiyo Hans van Pluijm ambaye kwa sasa atakuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo.

Lwandamina amesema kuwa atakuwa mkali kwa wachezaji wazembe kutokana na makubaliano aliyoingia na viongozi wa klabu hiyo ambayo alisema yanamlazimu kuwa mkali.

Pia amesema siku zote katika kazi yake ya ukocha amekuwa na mapenzi makubwa na wachezaji wake kwa sababu anaamini ndio watakaompa mafanikio na kusema katika hilo angependa kila mmoja kutimiza wajibu ili kwenda sawa na malengo yake.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia alisema kuwa anatambua Yanga ni timu kubwa yenye mashabiki wengi na kwa kupitia taaluma yake atahakikisha anaendeleza furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *