Serikali ya Zambia imeahirisha sherehe za kuapishwa Rais mteule wa nchi hiyo, Edgar Lungu hadi wakati mwingine baada ya chama kikuu cha upinzani cha Muungano wa Ustawi na Kitaifa (UPND) kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini humo.

Chama cha UPND kimewasilisha mashtaka mahakamani kikitaka kuhesabiwa tena kura zote za uchaguzi huo suala ambalo limeilazimisha serikali ya nchi hiyo kuahirisha zoezi la kuapishwa rais mteule Bw. Lungu.

Sheria za Zambia zinasisitiza kuwa, iwapo chama chochote kitawasilisha mashtaka mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi, rais mteule hawezi kuanza kazi rasmi.

Matokeo ya uchunguzi na uhakiki wa kura za uchaguzi wa rais wa Zambia yatatangazwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.

Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Rais Edgar Lungu wa chama tawala cha Patriotic Front (PF) alishinda uchaguzi huo kwa kujinyakulia asilimia 50.35 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Hakainde Hichilema wa chama cha upinzani cha UPND aliyepata asilimia 47.63 ya kura zote.

Lungu amemshinda mpinzani wake Hichilema ambaye ni mfanyabiashara tajiri kwa tofauti ya takribani kura laki mbili.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *