Mahakama Kuu jijini Dar es salaam, imesema muigizaji Elizabeth Michael (Lulu) ana kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma za kuuwawa kwa msanii Steven Kanumba , hivyo anatakiwa kujitetea.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Mahakama kuu baada ya kufunga kusikiliza ushahidi upande wa mashtaka na kumtaka muigizaji huyo kuanza kujiandaa kwa ajili ya kutoa utetezi wake.

Wakili wa Elizabeth, Peter Kibatala ambaye ndiye anayemtetea muigizaji huyo, aliomba muda wa dakika 40 ili wajiandae kufanya hivyo.

Baada ya Lulu kuanza kujitetea amesimulia jinsi ilivyokuwa siku ya tukio, Lulu amesema marehemu alikuwa akimpiga na panga baada ya kutokea ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi, alipomuona akiongea na simu.

Lulu amesema kuwa “Nilikuwa nataka kutoka ila marehemu ‘Kanumba’ alinikataza, alikuwa hataki nitoke, nilipomwambia natoka na marafiki zangu alinikimbiza na taulo na mimi nilikuwa naogopa kupigwa, mara nyingi alikuwa ananipiga kila akilewa na sio kwa akili zake, alipoona simu yangu inaita akahisi ni simu ya mwanaume akasema kwanini naongea na simu ya mwanaume mbele yake? Marehemu akaingia uvunguni akatoa panga akasema leo nakuua huku akinipiga na panga kwenye mapaja”,.

Lulu ameendelea kusimulia….”Marehemu alianguka mwenyewe na kujigonga kwa nguvu na kuinuka sehemu nyingine alikuwa kama anatapatapa, nilimwambia Seth kuwa Kanumba amedondoka na akajaribu kumuamsha hakuamka akasema anaenda kumuita daktari, alivyosema anaenda kumuita daktari na mimi nikaondoka nikiogopa anaweza akaamka akaanza kunipiga, niliondoka nikawasha gari kuelekea Coco Beach kutuliza akili”.

Pia amesema kuwa “Nilivyofika Coco beach meseji zilianza kusambaa kuniuliza kuwa nasikia Kanumba amefariki, nikampigia ‘Kidume’  ambaye ni rafiki yake Kanumba kumuuliza Kanumba yupo hospitali gani niende kumuona, akaniambia wewe usije hospitali, niambie uko wapi, tukakubaliana tuonane Bamaga, tulivyokutana Bamaga alikuwa kama anataka kuongea na mimi ghafla wakaja askari kunikamata”.

Pamoja na hayo muigizaji huyo ameithibitishia mahakama kuwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu (Steven Kanumba) kwa muda wa miezi minne kabla ya kukutwa na mauti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *