Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amemsimamisha kazi Afisa Mipango Miji wa Lindi, Castory Manase Nkuli.

Hatua hiyo imekuja baada ya kunyang`anya ardhi ya vijiji vya Ruvu na Mchinga hekari 4,000 na kumilikisha kampuni ya Azimio Housing Estate kinyume cha sheria ya Ardhi.

Lukuvi aligundua hayo baada ya kuona utaratibu wa umilikishaji wa ardhi haukufuatwa  na badala yake kuonekana kuwa na mianya ya rushwa kwa kuwa ardhi hiyo imehamishwa kutoka ardhi ya kijiji hadi kumilikishwa kwa kampuni ya Azimio ambapo kisheria ilitakiwa hati ya eneo hilo itoke kwa idhini ya Rais.

Afisa Mipango Miji huyo aligundulika kuwa na kosa la kughushi kwa kujifanya ni Afisa ardhi baada ya kuandika barua na kuisaini kwa niaba ya Afisa ardhi wakati yeye ni Afisa Mipango Miji ili kuimilikisha kampuni ya Azimio Housing Estate ambalo pia ni kosa kisheria.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji kutoka Wizara ya Ardhi Bi Immaculate Senje amesema kwamba utaratibu wa umilikishaji wa ardhi hiyo haukufuatwa ambapo kisheria ilitakiwa hati ya eneo hilo itoke kwa idhini ya Rais na baada ya Tangazo la Serikali na kuridhiwa na wana kijiji.

Katika ziara yake mkoani Lindi Lukuvi ametembelea ofisi za ardhi Lindi na kufanya ukaguzi katika Masijala za ardhi na kuangalia mfumo wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi.

Pia amewaagiza watendaji wa ardhi mkoani hapo kuhakikisha wanatoa hati kwa wakati na kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa kila mmiliki wa ardhi ili kuongeza pato la serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *