Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amefuta hati za viwanja 15 vilivyokuwa vinamilikiwa na Hermant Patel na kurejesha umiliki wake kwa serikali.
Inaelezwa kuwa viwanja hivyo vilipatikana kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwanza jana, Lukuvi amesema anaishukuru ofisi ya ardhi Kanda ya Ziwa kwa kutekeleza agizo la kufuta umiliki wa hati 15 za Patel.
Amesema mtu huyo alipata hati hizo kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia hati ya uraia pacha wa Tanzania na Uingereza.
Pia Waziri alisema awali ilidhaniwa Patel anamiliki hati tano za viwanja lakini kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) imegundulika ana hati 15 alizozipata kwa njia ya udanganyifu kwa kuwa na uraia wa nchi mbili.
Vile vile Lukuvi amewaonya watu wote wenye tabia kama ya Patel ya kutumia hati za kuishi nchini zenye uraia wa nchi mbili, ambao walifanya udanganyifu na wanamiliki ardhi kama raia wa Tanzania wajisalimishe vinginevyo watashughulikiwa na kunyang’anywa ardhi wanazozimiliki.