Mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amefunguka sababu ya kutovaa sare za chama hicho katika mikutano au shughuli za kichama.
Lowassa amesema kuwa “Si kweli kuwa sivai sare cha CHADEMA, hata nilipokuwa CCM nilikuwa nashona shati la rangi moja ama kijani au njano kisha naweka nembo maalumu ya chama, vivyo hivyo hata CHADEMA naweka nembo maalum.
Lowassa ambaye ni waziri mkuu mstaafu amesema kuwa “Na jambo kubwa hapa ni kuwa, nisihukumiwe kwa kuvaa au kutokuvaa sare za CHADEMA lakini kwa matendo yangu.”
Pia amesema kuwa sare si jambo kubwa sana kwani mtu anaweza kuvaa sare na bado akawa si mmoja wenu. Unaweza kukuta mtu kavaa nguo za kijani lakini kiukweli moyoni si wa CCM
Lowassa amesema alipomaliza Chuo Kikuu alikwenda jeshini na kwa muda wote huo alikuwa akivaa magwanda hivyo alishavaa vya kutosha, na umri wake kwa sasa si wa kuvaa tena.