Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amemjia juu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi  na kusema Waziri huyo hana sifa za kuendelea kuwepo katika wizara hiyo kutokana na kuwa na majibu mepesi kuhusu matukio ambayo yanagharimu maisha ya watu.

Lema amesema hayo leo alipokuwa jijini Arusha akiongea na waandishi wa habari na kusema amesikitishwa sana na majibu ya Waziri Mwigulu Nchemba kuhusu sakata la miili ya watu kuokotwa baharini na sakata la shambulio la Tundu Lissu pamoja na kupotea kwa Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Lema amesema kuwa “Mwigulu Nchemba amenisikitisha sana kwa kauli zake alizokuwa anatoa na sidhani kama anastahili kukalia ile ofisi hata kwa masaa 12 na ni wito wangu kwa Mhe. Rais Magufuli na naamini itakuwa hivyo hawezi kumuacha Waziri kama huyu kwenye ofisi ya serikali inayoshughulika na mambo ya ulinzi na usalama wa watu, matumaini yangu yupo hapo kwa muda tu.

Aidha Mbunge huyo amesema kuwa kitendo cha Waziri Mwigulu Nchemba kusema gari ambayo alikuwa anailalamikia Mbunge Tundu Lissu na yeye kusema gari hiyo imeonekana Arusha na haijawahi kutoka Arusha bila kuchukuliwa hatua yoyote ni jambo ambalo linaibua maswali mengine na kufanya wazidi kukosa imani na jeshi la polisi kuhusu kuchunguza sakata la Tundu Lissu.

Lema amesema kuwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani hajui juu ya Ben Sanane kama amekufa au yuko hai polisi hawa tunasema hawawezi kuchunguza sakata la shambulio la Tundu Lissu ndiyo maana tunataka uchunguzi kutoka nje ya nchi waje kusaidia jambo hili.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *