Kaimu Rais wa Ab Dhabi,  Mohamed bin Zayed Al Nahyan ameahidi kuendelea kuimarisha uhusiano baina ya nchi hiyo na Tanzania katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ahadi hiyo ya Mrithi wa Mfalme wa Abu Dhabi imetolewa Ikulu jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mohamed Al Suwaidi aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli, ambaye naye alikaribisha taifa hilo ujenzi reli ya kati.

Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi unashirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na katika mazungumzo ya jana, mkurugenzi huyo, Al Suwaidi alionesha nia zaidi ya kushirikiana na Tanzania. Maeneo ya ushirikiano yaliyopewa kipaumbele na mkurugenzi huyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli na barabara, usafiri wa anga na madini.

Pamoja na kumshukuru mrithi huyo wa Mfalme, Rais Magufuli ameialika nchi hiyo kupitia mfuko wake huo na wadau wengine wa maendeleo kuwekeza nchini katika miradi ya maendeleo.

Miradi hiyo ni ujenzi wa bandari, ujenzi wa viwanda, kilimo, uvuvi, gesi na kushirikiana katika ujenzi wa reli ya kati ambayo itazinufaisha nchi nyingine saba za Afrika Mashariki na Kati ambazo hazina bandari.

Ameongeza kuwa,Tanzania imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali na bado ushirikiano kama huo unahitajika kwa sababu maeneo ya uwekezaji ni mengi, mfano kwenye ujenzi wa reli.

Aidha, Rais Magufuli aliutaka mfuko huo kufupisha muda unaotumika katika mchakato wa kuanza utekelezaji wa miradi ili kuharakisha matokeo yake na manufaa kwa wananchi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *