Mbunge wa Ubungo (Chadema) Said Kubenea ameondolewa mashataka ya uchochezi na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na upungufu  katika hati ya mashtaka kwenye kesi hiyo.

Hata hivyo, mara baada ya kuondolewa kwa hati hiyo ya mashtaka, Kubenea alichukuliwa na maofisa wa polisi hadi Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa mahojiano ambapo inadaiwa baada ya mahojiano aliachiliwa.

Uamuzi huo umetolewa leo mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, baada ya Wakili wa Serikali, Derrick Mkabatunzi,  kueleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya uamuzi.

Katika uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema anakubaliana na pingamizi zilizowasilishwa na upande wa utetezi kupitia Wakili Jeremiah Mtobesya kuwa hati ya mashtaka ina mapungufu na ilikuwa na utata kiasi kwamba haiendani na kosa analoshitakiwa mshtakiwa.

Kubenea anatuhumiwa kuandika kichwa cha habari ambacho kinadaiwa kilikuwa na  uchochezi,  kilichosema:  ‘Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?’ ambacho kwa mujibu wa hakimu alidai kichwa hicho hakina kosa lolote  na upande wa mashtaka ulipaswa kuandika maneno yanayodhaniwa kuwa ni ya uchochezi.

Hakimu alifafanua  kuwa hati hiyo ina mapungufu kwa sababu haielezi ni namna gani mshtakiwa ametenda kosa na  hivyo ingesababisha mshtakiwa ashindwe kujitetea.

Aliendelea kueleza kuwa  hati ya mashtaka imeondolewa mahakamani, isipokuwa jamhuri bado wanayo nafasi ya kufungua kesi nyingine kwa mujibu wa sheria ya magazeti na ya makosa ya jinai.

Awali katika kesi hiyo wakili  Mtobesya  alidai kuwa hati hiyo ya mashtaka  ina mapungufu na inakinzana na matakwa ya sheria ya magazeti na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, hivyo akiomba mahakama iifutilie mbali na kumuachia huru Kubenea.

Wakati huohuo, Wakili Mkabatunzi alidai kuwa hati ya mashtaka inayomkabili Kubenea ipo sahihi na kwamba imekidhi matakwa ya kisheria  na akaongeza kuiomba mahakama itupilie mbali pingamizi lao.

Katika kesi hiyo, Kubenea anadaiwa kuwa  alifanya kosa hilo Julai 25, 2016 ambapo alichapisha habari ama makala ambayo ingeweza kusababisha hofu kwa jamii ama kuharibu hali ya amani.  Chapisho hilo lilitolewa  kwenye gazeti la Mwanahalisi  la Julai 25-31, 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *