Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla amegundua kiwanda cha kutengeneza konyagi feki jijini Dar es Salaam.

Dk. Kigwangalla ameshirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA) na Tume ya Ushindani pamoja na Jeshi la Polisi kunasa kiwanda hicho bubu.

Kiwanda hicho kilinaswa kwenye nyumba ya mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Koku maarufu ‘Mama Kareem’ eneo la Sinza Kijiweni,  Dar es Salaam kikitengeneza konyagi, viroba na pombe kali ya  smirnoff.

Katika kiwanda hicho pia kulikutwa malighafi mbalimbali zinazotumika kutengenezea bidhaa hizo likiwamo dumu kubwa lililokuwa  limejaa gongo.

Vingine ni  dumu la spirit lita 20, chupa tupu  na zilizojazwa kwa ajili ya kusambazwa, vizibo vya chupa za konyagi na smirnof pamoja na  vifungashio vya aina mbalimbali.

Taarifa ya Dk. Kigwangala aliyoisambaza kupitia mitandao ya  jamii jana, ilisema Jeshi la Polisi limewatia mbaroni watu wawili ambao inasemekana ni wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *