Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Hakainde Hichilema pamoja na naibu wake wamefikishwa mahakamani nchini humo ambapo wameshtakiwa makosa ya uchochezi wa maasi pamoja na kufanya mkutano kinyume cha sheria.

Viongozi hao wote wamekanusha mashtaka hayo, na wakaachiliwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana kwa kulipa $2,500 (£2,000) kila mmoja.

Viongozi hao wa upinzani, Hichilema na naibu wake Geoffrey Bwalya Mwamba walikamatwa siku ya Jumatano na wakalala selo mpaka siku ya jana.

Mashtaka hayo yanahusiana na hotuba ya kushtukiza ambayo Hichilema aliitoa Septemba 26 katika mji wa Mpongwe katikati mwa nchi hiyo.

Hichilema alishindwa kwenye uchaguzi wa urais mwezi Agosti na Rais Edgar Lungu ingawa amelalamika kwamba kulitokea udanganyifu.

Kesi ya viongozi hao wa upinzani inatarajiwa kuendelea tena ifikapo Oktoba 19 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *