Wafungwa wengine wametoroka kutoka gerezani siku mbili baada ya zaidi ya wafungwa 3,000 kutoroka kwenye gereza kuu nchini Jamhuri ya Demokrasia Congo.
Wafungwa 60 wanadaiwa kutoroka kutoka jela ya Kasangulu, kilomita 40 kutoka mji mkuu Kinshasa.
Gereza hilo linapatikana katika eneo ambalo ni ngome ya madhehebu ya Bundu Dia Kongo.
Katika kisa cha awali, ambapo wafungwa wengi walitoroka gereza kuu mjini Kinshasa, kiongozi wa madhehebu hayo aliyekuwa amezuiliwa anadaiwa kuwa miongoni mwa waliofanikiwa kutoroka baada ya watu wenye silaha kuvamia jela hiyo.
Kwa sasa, maafisa wa serikali watafakari uwezekano wa kutuma jeshi kulinda magereza yote nchini humo.