Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekemea tabia ya baadhi ya viongozi kulumbana na kuibua migogoro ambayo hurudisha nyuma maendeleo ya Chama hicho.

Kauli hiyo imesemwa na katibu mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana wakati akizindua Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo la Mpendae Mjini Unguja, ambao umeanzishwa na Mbunge wake, Salim Hassan Turky.

Kinana amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa majimbo ya uchaguzi, kulumbana na kuibua migogoro ambayo hurudisha nyuma maendeleo ambayo yanatokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

Katibu Mkuu huyo alisema Chama hakitosita kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi wa majimbo, ambao wataendekeza majungu na kusababisha malumbano na hatimaye kurudisha nyuma malengo ya wananchi kupata maendeleo.

Kinana amesema amefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa Turky kwa kuwawezesha wananchi, ikiwemo wajasiriamali kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kupambana na umaskini.

Amesema kupambana na umasikini na kuwawezesha wanawake katika vikundi vya uzalishaji mali, ndiyo mikakati na malengo ya CCM kwa ajili ya kupambana na umaskini.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *