Kikosi maalum cha jeshi la Ivory Coast ambacho kinaripoti moja kwa moja kwa rais wa nchi hiyo kilichopo kwenye mji wa Adiake uliopo kusini – mashariki mwa nchi hiyo imeanzisha mgomo.

Wakazi wa eneo hilo lililopo karibu na mpaka wa nchi ya Ghana wamelazimika kusalia majumbani mwao huku maduka na shule zikilazimika kufungwa.

Chanzo cha mgomo huo kwa mujibu wa wanajeshi wa kikosi hicho ni kuibiwa sehemu ya mishahara yao na makamanda wao.

Tukio hili limejitokeza ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu wanajeshi wa kawaida nao kuanzisha mgomo na kufanya vurugu kwa madai ya kukosa mishahara kwa muda mrefu na hali mbaya ya maisha yao.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu mmoja wa walimu wa shule ya sekondari aliyekaririwa akisema:

‘Milio ya risasi ilianza kusikika mapema kwenye kambi ya kikosi maalum kisha mji ukaanza kutaharuki baada ya kuwaona wanajeshi hao wakiondoka kwenye kambi hiyo’.

Shirika la BBC limeripoti kuwa tayari ujumbe wa katibu mkuu wa serikali umeshaenda kwa helikopta kwenye kambi hiyo kwaajili ya kufanya mazungumzo na wanajeshi hao wanaokadiriwa kufikia 800.

Mwanajeshi mmoja amekaririwa na chombo cha habari cha nchi hiyo akidai kupokea $80 ya mshahara wake wa mwezi ambao ni $400.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *