Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imehairisha kesi inayomkabili staa wa Bongo Movie, Wema Sepetu.

Kesi hiyo imeharishwa hadi Agosti 15 mwaka huu kutokana na shahidi upande wa serikali kutofika mahakamani kwa kile kilichoelezwa kuwa amepata dharura.

 Agosti 1, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri aliyefahamika kwa jina la Elias Mulima kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali akisoma ripoti ya uchunguzi alisema mahakamani hapo kuwa mkojo wa Wema baada ya kupimwa ulikutwa na chembechembe za bangi.

 Kwa upande wa wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alisema ripoti hiyo iliyosomwa na Mulima ina upungufu mwingi wa kisheria. Baada ya kutokea malumbano hayo Hakimu Mkazi Simba aliwaomba mawakili wa pande zote mbili kuridhia apate muda wa kuipitia taarifa hiyo ya Ofisi ya Mkemia Mkuu ili itakapoendelea aweze kuitolea ufafanuzi.

 Pia mahakama hiyo imepokea maelezo ya Mkemia Mkuu na fomu iliyotakiwa kuambatanishwa kwenye ripoti ya mkemia ya mwanzo ambayo Wakili Kibatala alikuwa akipinga kutoambatanishwa wakati huo hakimu ameeleza kuwa haina umuhimu.

Wema na wenzake wanashtakiwa kwa kosa la kukutwa na kutumia bangi ambapo kesi hiyo itaendelea tena Agosti 15 na 16 2017.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *