Kesi ya kupinga baadhi ya vipengele vya Sheria ya huduma za vyombo vya habari imefunguliwa na Baraza la Habari Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ) ambayo ofisi zake ziko katika jengo la Mahakama ya Rufani, jijini Dar es Salaam chini ya mawakili Fulgence Massawe, Donald Deya, Jenerali Ulimwengu, Jebra Kambole, Francis Stolla na Mpale Mpoki ambao wanaziwakilisha taasisi hizo.

Katika kesi hiyo, washirika hao wanataka baadhi ya vifungu kwenye sheria hiyo ambavyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza vifutwe kwa madai kuwa vinakiuka matakwa ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ibara za 6(d) na 7(2).

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mkajanga amesema kwa mujibu wa kifungu cha 8 (1) c , Tanzania inapaswa kuchukua hatua kuhakikisha haki zote zinazotajwa katika mkataba huo zinafuatwa na kutekelezwa.

Amesema Tanzania iliridhia mkataba huo Julai 7, 2000 chini ya kifungu namba 23 cha mkataba huo, mahakama imepewa mamlaka ya kutafsiri mkataba huo na kuhakikisha nchi wanachama wanaufuata na kuusimamia.

Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge Novemba 5 mwaka jana na baadaye kuidhinishwa na Rais Magufuli Novemba 16 mwaka jana.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *