Serikali ya Kenya imesema itapunguza mishahara ya wabunge na maafisa wakuu kutokana na viwango vya juu vya mishahara yao kusababisha migomo ya wafanyakazi wa sekta nyingine.

Hayo yamesemwa na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta alipokuwa nahutubia kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Taifa na Baraza la Senate katika hotuba yake ya mwisho ya kipindi chake cha kwanza madarakani.

Hotuba ya Rais huyo imesheheni majibu ya maswali yanayoulizwa na upinzani kila siku kuanzia ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, kuzorota kwa huduma za afya, elimu na usalama.

Kwa upande mwingine Rais Uhuru amejivunia kupungua kwa visa vya mashambulizi ya kigaidi nchini, kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama na ukuaji wa uchumi ambao amesema umekuwa juu ya kiwango cha makadirio ya taasisi za kimataifa cha 3% kwa Mwaka.

Huku zikiwa zimesalia siku 145 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Rais Kenyatta ametumia fursa ya hotuba hiyo kujipigia kampeni ili aweze kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili.

Rais Kenyatta amesema kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha uchaguzi huru na haki na kuiomba Idara ya Mahakama kutotatiza matayarisho ya uchaguzi ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *