Kaya  6,249 katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, zitanufaika na ruzuku kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika kipindi cha Septemba hadi Oktoba, mwaka huu.

Mratibu wa Tasaf wilayani humo Bernard Gishuli, amesema hayo ofisini kwake wakati akitoa taarifa ya kuanza kwa kazi ya uhawilishaji fedha za ruzuku kwa kaya masikini. Gishuli alisema Sh milioni 230.5 kutoka mfuko huo, zinatarajia kuwasaidia walengwa kipato ili kujikwamua kimaisha.

Ametaja idadi ya vijiji vinavyonufaika na fedha hizo kuwa ni 78, na kwamba fedha zinazotolewa na TASAF III zinatoa fursa kwa kaya hizo kupata huduma za kijamii.

Mratibu huyo amesema mfuko huo unatoa ruzuku za aina mbili, ya msingi inayotolewa kwa kaya zote masikini zilizoandikishwa kwenye mpango na nyingine ni ya utimizaji masharti ambayo hutolewa kwa kaya zenye watoto wanaotakiwa kwenda shule na vituo vya kutolea huduma za afya.

Kishapu ni miongoni mwa halmashauri za wilaya 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba zinazotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf III) ili kuongeza kipato na fursa za kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *